Katika kikao hicho Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alizungumzia masuala kadhaa muhimu ambayo yanaweza kugawanywa katika nukta na mihimili mitano muhimu.
Muhimili wa kwanza ni uungaji mkono wa dhati wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa uthabiti, maendeleo na usalama wa Iraq. Iraq ina mpaka wa pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,500. Siasa za kudumu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Iraq baada ya kusambaratika utawala wa Baathi uliokuwa ukitawala nchi hiyo, ni kuunga mkono utulivu, usalama na maendeleo yake pamoja na kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali. Katika kikao chake na Waziri Mkuu as-Sudani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba maendeleo ya Iraq na kufikia nafasi yake ya juu na stahiki ni kwa maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu na kubainisha kuwa: “Mtazamo wetu kuhusu usalama wa Iraq ni kwamba iwapo upande wowote utakusudia kuvuruga usalama wa nchi hiyo, tutasimama imara katika kutetea na kuilinda Iraq."
Mhimili wa pili muhimu katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ni kusisitiza juu ya ulazima wa kuwepo mafungamano na umoja wa makundi yote ya Iraq. Kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, Iraq ni nchi iliyoendelea zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu katika uwanja wa maliasili na wasomi, utamaduni, historia na ustaarabu, lakini pamoja na hayo, bado haijaweza kufikia nafasi yake stahiki na halisi katika uwanja huo. Hitilafu za ndani zimekuwa sababu muhimu ya kudumaa na kutoendelea Iraq katika miongo miwili iliyopita. Kwa msingi huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba moja ya mahitaji ya msingi ya Iraq kwa ajili ya kufikia nafasi yake halisi, ni kuwepo mshikamano na umoja wa makundi ya nchi hiyo.
Mhimili wa tatu katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu hapo jana alasiri, ni kuwekwa wazi msimamo wa maadui dhidi ya Iraq na maslahi yake. Katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono maendeleo ya Iraq, baadhi ya nchi zinaona kwamba usalama na maendeleo ya nchi hiyo haziwiani na maslahi yao. Kwa upande mmoja, mtazamo wa maadui wa Iraq ni kwamba ni nani na ni kundi gani litakalokuwa madarakani, na kwa upande mwingine, wanaitazama Iraq yenye nguvu na iliyostawi kama mshindani wao na kwa hivyo hawataki hilo lithibiti. Kwa hiyo, katika mazungumzo yake na Shia as-Sudani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Maendeleo ya Iraq yana maadui ambao huenda wasioneshe uadui wao hadharani, lakini hawaikubali serikali kama yako..."
Mhimili wa nne, ambao kwa namna fulani huenda ukawa ndio mhimili muhimu zaidi katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, ni sisitizo la kuwepo usalama katika mipaka ya Iran na Iraq. Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wamekuwa wakitumia mipaka ya maeneo ya kaskazini mwa Iraq kuhujumu usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, jambo ambalo limeonekana wazi katika machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, ambapo makundi ya kigaidi yenye makao yake kaskazini mwa Iraq yamekuwa na nafasi muhimu katika machafuko hayo kwa kujipenyeza ndani ya ardhi ya Iran.
Utepetevu wa serikali ya Iraq katika kukabiliana na makundi ya kigaidi yaliyoko katika mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo umekosolewa na Kiongozi Muadhamu. Akirejea maneno ya as-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, kwamba kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, hataruhusu kundi lolote kutumia ardhi ya Iraq kwa ajili ya kuvuruga usalama wa Iran, Kiongozi Muadhamu amesema: “Kwa bahati mbaya, hayo yanafanyika katika baadhi ya maeneo ya Iraq na njia pekee ya kutatua tatizo hilo ni kwamba serikali kuu ya Iraq inapasa kupanua mamlaka na udhibiti wake kwenye maeneo hayo pia."
Mhimili wa tano katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu umekuwa ni ulazima wa kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa huko nyuma kati ya nchi mbili hizi hususan katika nyanja za kiuchumi. Kiwango cha mabadilishano ya biashara kati ya nchi hizi kwa sasa ni cha thamani ya dola bilioni 12, katika hali ambayo pande mbili tayari zimekubaliana kuongeza kiwango hicho hadi dola bilioni 20, jambo ambalo halijafuatiliwa inavyopaswa hadi sasa. Bila shaka, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kizingiti kikubwa kinachovuruga shughuli za kufikiwa lengo hilo. Katika kikao chake na Shia as-Sudani, kiongozi wa Mapinduzi ameashiria mapatano yaliyofikiwa jana kati ya Rais wa Iran na Waziri Mkuu huyo wa Iraq na kusema: "Katika vipindi vilivyopita, mazungumzo na maelewano mazuri yalifikiwa, lakini ni sehemu ndogo tu ya maelewano hayo ndiyo imetekelezwa kufikia sasa. Kwa hivyo, inabidi tuelekee upande wa kutekeleza maelewano yote, hasa katika uwanja wa ushirikiano wa kiuchumi na ubadilishanaji wa bidhaa na mawasiliano ya reli.
342/